Skip to main content
News and Events

Balozi Mteule wa Jamhuri ya Cyprus, awasilisha Nakala za Hati za Utambulisho

Tarehe 27 Machi, 2025 Balozi Mteule wa Jamhuri ya Cyprus mwenye makazi yake Nairobi Kenya, Mhe. Savvas Viadimirou amewasilisha nakala ya hati za utambulisho kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Dennis Londo (Mb).

Akipokea nakala za hati hizo kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, katika Ofisi ndogo za Wizara, jijini Dar es Salaam Mhe. Londo ampongeza Mhe. Viadimirou kwa kuaminiwa na kuteuliwa kuiwakilisha nchi yake hapa nchini na kuahidi kuwa Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, itampatia ushirikiano wakati wote ili kumwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Mhe. Londo amesema Tanzania na Jamhuri ya Cyprus zimekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia tangu wakati wa Uhuru, uliojengwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kuendelea kukua na kuimarika mpaka sasa chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.